Mbunge mteule wa Jimbo la Monduli Mkoani Arusha Julius Kalanga (CCM) akinyanyua juu cheti cha ushindi wa nafasi hiyo baada ya kukabidhiwa.
.............................................................
Mgombea Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Monduli Mkoani Arusha Ndugu Julius Kalanga atangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi huo Bw. Steven Ulaya kuwa mshindi wa Uchaguzi mdogo kwa kupata kura 65,714 sawa na asilimia 95% ya kura zote zilizopigwa kwenye uchaguzi huo.
Ulaya akitangaza matokeo ya uchaguzi huo saa 6:30 usiku alisema shughuli za kupiga kura zilienda vizuri hadi hatua ya kutangazwa na kulikuwa na amani na usalama wa kutosha.
Aliwataja wagombea wengine ni Yonas Laizer wa Chadema aliyepata kura 3,187 ,Wilfred Mlay wa ACT Wazalendo kura 144, Feruz Juma wa NRA alipata kura 45, Simon Ngilisho wa Demokrasia Makini alipata 35, Omary Juma wa DP kura 34, mgombea wa ADA-Tadea, Francis Ringo kura 21 na Elizabeth Salewa wa chama cha Wakulima kura 16.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Kalanga aliwashukuru waliomchagua na kuahidi atawatumia kwa nguvu zote bila kubagua vyama.
Kalanga alisema ataendelea pale alipoishia na kutaja vipaumbele vyake ni kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa ajili ya matumizi ya watu na mifugo.
“Kwa nguvu zote nitashughulikia utatuzi wa migogoro ya ardhi inayokwamisha shuguli za maendeleo hapa kwetu Monduli,” alisema Kalanga.
Alisema hizo ndizo ajenda zake muhimu atakazozisimamia kikamilifu akishirikiana na viongozi wenzake ili kuhakikisha Monduli inabadilika.
Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Manyara Ester Mahawe (CCM) alisema CCM imepata ushindi kutokana na kampeni za kistaarabu ilizofanya sanjari na kueleza mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi kifupi cha uongozi wa Rais John Magufuli.
“Wananchi wa Monduli wametupa heshima kubwa kwa kuirudisha tena CCM madarakani kwani miaka yote CCM ilikuwa inatawala Monduli ila upepo na mafuriko yaliwabeba,” alisema Mahawe.



























