Serikali imesema inatarajia kuweka jiwe la msingi mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu kwa ajili ya ujenzi wa gati kubwa katika bandari ya Mtwara ambapo awali ujenzi wake ulishindikana kufanyika kutokana na Mkandarasi wa awali kudai malipo makubwa.
Akizungumza mara baada ya kukagua bandari hiyo mkoani Mtwara, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema nia ya serikali ni kujenga gati nne katika bandari hiyo ambapo kwa kuanza itajenga gati moja.
“Tumempata Mkandarasi ambaye atajenga gati moja kwa Shilingi milioni 70, hivyo gharama za ujenzi zitapungua ukilinganisha na mkandarasi wa awali aliyetaka kulipwa bilioni 100 kwa ujenzi wa gati moja”, amesema Waziri Mbarawa.
Profesa Mbarawa ameongeza kuwa ujenzi wa gati hilo utapelekea meli kubwa zenye urefu wa mita 300 kuweza kutia nanga bandarini hapo na hivyo kufungua fursa za kiuchumi na ajira kwa wakazi wa mkoa huo.
Aidha, amewataka watendaji wa bandari hiyo kushirikiana na Mkandarasi huyo ili kuweza kufanikisha ujenzi huo kukamilika kwa haraka na kwa viwango vilivyomo kwenye mkataba huo.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa bandari hiyo, Abilahi Salim, amesema kuwa ujenzi wa gati hilo utahusisha upanuzi wa mlago ambapo utachimbwa zaidi ili kurahisisha meli kubwa kuingia kwa urahisi.
Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa amezungumza na Watumishi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake na kuwataka kufanya kazi kwa uadilifu, ubunifu na kuboresha mawasiliano baina ya viongozi wa juu wa taasisi hizo na watumishi lengo likiwa ni kufikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano katika utoaji huduma na uboreshaji wa miundombinu bora na ya kisasa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mkoa wa Mtwara, Bw. Abilahi Salim (hayupo pichani), kuhusu ujenzi wa gati kubwa litakalojengwa katika bandari hiyo hivi karibuni.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa(aliyenyoosha mkono), akifafanua jambo kwa Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),mkoa wa Mtwara, Bw. Abilahi Salim(kulia kwa Waziri) wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya bandari hiyo, leo.

Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), mkoa wa Mtwara, Bw. Abilahi Salim akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa(katikati) baadhi ya makontena yaliyokuwa yamepaki bandarini hapo wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya bandari hiyo, leo.

Muonekano wa bandari ya Mtwara ambapo Serikali inatarajia kujenga gati kubwa katika bandari hiyo hivi karibuni.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mtwara, kuhusu ujenzi wa gati kubwa litakalojengwa katika bandari ya Mtwara hivi karibuni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni