Meneja Kitengo cha kumaliza
Malaria Zanzibar Abdalla Suleiman Ali akifungua mkutano wa siku moja wa
wadau wa Malaria uliofanyika Hoteli ya Ocean View Kilimani Mjini
Zanzibar.
Afisa uchunguzi wa vimelea vya
Malaria Zanzibar Safia Mohammed Ali akiwasilisha mada ya njia za
kukabiliana na maradhi hayo katika mkutano wa wadau wa Malaria
uliofanyika Hoteli ya Ocean View Kilimani .
Naibu Meneja wa ZAMEP Faiza
Bwanakheri akitoa mada ya njia za kudhjibiti na kumaliza Malaria
Zanzibar katika mkutano wa wadau wa Malaria uliofanyika Hoteli ya Ocean
View.
Baadhi ya wadau wa Malaria
walioshiriki mkutano wa siku moja katika Hoteli ya Ocean View
wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa katika mkutano huo.Picha na
Makame Mshenga.
Meneja Kitengo cha kumaliza
Malaria Zanzibar Abdalla Suleiman Ali amesema mashirikiano ya pamoja
yanahitajika kuanzia ngazi ya shehia hadi Taifa katika kufikia malengo
ya kumaliza maradhi hayo nchini.
Alisema kazi ya kumaliza Malaria
Zanzibar sio kazi rahisi kama inavyofikiriwa na watu wengi lakini nguvu
za pamoja za wadau mbali mbali wa ndani na nje ya nchi zinahitajika.
Meneja Abdalla Suleiman alieleza
hayo katika mkutano wa siku moja wa wadau wa Malaria uliozungumzia hali
ya ugonjwa huo ulivyo hivi sasa na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na
Serikali kupitia kitengo hicho uliofanyika Hoteli ya Ocean View Kilimani
Mjini Zanzibar.
Alisema pamoja na Zanzibar kupata
mafanikio makubwa katika kukabiliana na Malaria bado zipo baadhi ya
sehemu maradhi hayo yanaendelea kujitokeza na ni vigumu kukabiliana nayo
kwa vile kunahitajika ufuatiliaji wa karibu kwenye familia zinazotoka
wagonjwa hao.
Aliongeza kuwa kabla ya
kuanzishwa kitengo cha kumaliza Malaria, Zanzibar ilifikia kuwa na
wagonjwa zaidi ya laki tatu kwa mwaka lakini hivi sasa wagonjwa wa
malaria hawazidi elfu nne kwa mwaka.
Alisisitiza kuwa lengo la Wizara
ya Afya kupitia Kitengo cha kumaliza Malaria ni kuhakikisha kuwa ifikapo
mwaka 2022 Zanzibar hakuna mtu anaeugua Malaria.
Akitoa mada ya hali ya Malaria
ilivyo hivi sasa, Ofisa wa Kitengo hicho Wahida Shirazi alisema Kisiwa
cha Unguja kunawagonjwa wengi zaidi wa maradhi hayo ukilinganisha na
Pemba na Wilaya ya Kati inaongoza kwa wagonjwa wengi ikifuatiwa na
Wilaya za Magharibi.
Alikumbusha kuwa Wilaya ya Chake
Chake inaongoza kwa kuwa na wagonjwa kidogo zaidi wa Malaria na baadhi
ya shehia za Wilaya hiyo hazijatoa mgonjwa hata mmoja kwa kipindi cha
mwaka mmoja.
Hata hivyo Ofisa huyo alisema
Kitengo cha kumaliza Malaria Zanzibar kimegundua wagonjwa wengi wa
malaria hivi sasa ni wenye tabia ya kusafiri mara kwa mara nje ya
Zanzibar na wanaamini wanapata ugonjwa huo wakati wa safari zao.
Akizungumzia umuhimu wa kutumia
vyandarua katika kupambana na Malari Afisa wa Kitengo hicho Mwinyi
Khamis alisema iwapo vitatumika vizuri vinaepusha maradhi hayo kwa
asilimia sitini hivyo amewashauri wananchi kuendelea kuvitumia
kikamilifu.
Baadhi ya wadau walioshiriki
mkutano huo walikishauri kitengo cha kumaliza mlaria kutoa elimu zaidi
kwa wananchi wanaokataa nyumba zao kupigiwa dawa badala ya kuviachia
vyombo vya dola kutumia nguvu kukamililsha kazi hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni